Header Ads

test

KUFUNGA si kazi,kazi kuilinda funga

1)Kuna mingi mitihani,wafungaji twapitia
Kila alie makini,haya alishasikia
Na kuyaona machoni,ama alishuhudia
Kufunga mbona si kazi,kazi kulinda swaumu.

2)Unatembea mjini,macho umejinamia
Mdada aja pembeni,vinguo kajivalia
Vaishia mapajani,mbeleyo akatizia
Kufunga mbona si kazi,kazi kulinda swaumu.

3)Simu yako mkononi,habari watafutia
Ingia mtandaoni,maovu washuhudia
Hawana haya usoni,picha chafu watupia
Kufunga mbona si kazi,kazi kulinda swaumu.

4)Wafika zako kazini,watu wana kutania
Usipokuwa makini,Funga wajiharibia
Welewi ufanye nini,bora kimya jikalia
Kufunga mbona si kazi,kazi kulinda swaumu.

5)Wapita zako sokoni,futari jinunulia
Hakuna wanazuoni,watu wajitukania
Wala shima hawaoni,shimo wanajichimbia
Kufunga mbona si kazi,kazi kulinda swaumu.

6)Mchana wa Ramadhani,yapo mengi yatokea
Jua Kali hadharani,madhambi yalobobea
Bila hata samahani,watu wanajitendea
Kutunga mbona si kazi,kazi kulinda swaumu.

 SHAIRI-KUFUNGA SI KAZI
MTUNZI-Idd Ninga,Arusha
+255624010160

Hakuna maoni