Header Ads

test

MAPIGANO NDANI YA FAMILIA (ushairi na hisia)


Ndani ya nyumba tena kwa siku ya leo kumezuka kizaa zaa,nghuo kuchanika nguo kupasuka.
wanafamilia kila mmoja kasusa hataki tena kazi za nyumbani na wanaamua kumuachia dada wa nyumbani au kile kilugha cha wenzetu hause geli (dah nilivyoandika sasa)
je nini kitajiri ?
ungana nami katika sehemu hii ya USHAIRI NA HISIA ili kujua nini kitatokea.


                                             SEHEMU YA KWANZA.
 BABA- haya wanangu nimewaita hapa ili mnieleze ni kwanini kile mmoja hapa tukimuambia afanye afanye kazi za nyumbani hataki au mnataka mama yenu ndio awafanyie.

KALIZA-Hapana baba mimi naona hizi kazi za nyumbani zinatuchosha sana na kutupotezea muda yani kila siku ni kutunga tu ni kutunga tu inamaana hakuna kazi nyingine ?
BABA-unaongea nini wewe ?
KALIZA-Ndio baba mimi sitaki kutunga tena
BABA-unataka kufanya nini ?



KALIZA-Najaza madaftari,mizani vina napanga.
Nakesha natafakari,tungo ije kuwakonga.
Ninajiona hodari,mnavyonita malenga.
NINAACHA USHAIRI,NAANZA KUTUNGA SHANGA.
2
Naambulia sifuri,kila kukicha majanga.
Moyo umenisha mori,madeni yamenizonga.
Sina pesa ya sukari,ninakopa hadi unga !!
SITUNGI TENA SHAIRI,SASA NINATUNGA SHANGA.
3
Shabiki wangu kwaheri,mkono leo napunga.
Mpenzi wa mashairi,mlango nimeufunga.
Nazidi kuwa fakiri,kwa misifa ya kijinga.
NIMEACHA USHAIRI,KALIZA NAUZA SHANGA.
4
Naenda kwa wanawari,kina mama na wakunga.
Wao hutoa dolari,kuzigharamia nyonga.
Ni mila na desturi,si rahisi kuzitenga.
SIYATUNGI MASHAIRI,SASA NINATUNGA SHANGA.
5
Wazee wanasihiri,wasanii na waganga.
Kila palipo tunguri,au jini kulipunga.
Mzigo upo tayari,agizeni manyakanga.
HAULIPI USHAIRI,NIBORA NITUNGE SHANGA.
6
Nawe kaka jemedari,hakika sijakutenga.
Nunua japo kwa siri,si vibaya ukihonga.
Hauna hela ya gari,mzawadie kishanga.
HII ND'O YANGU DHAMIRI,NIMESHINDWA KUJIVUNGA.
                                                                 Kaliza Bakari


BABA-yani wewe kweli umechanganyikiwa,yanii hi kazi alifanya babu wa mababu zako halafu we leo unataka kuacha eti ukauze shanga,hizo shanga zitakusaidia nini ?

KALIZA-ndio baba mimi nimeamua hivyo na hakuna wa kunipangia
BABA-Kisamvu unamsikia mdogo wako anachosema
KISAMVU-mdogo wangu sikia nikwambie kitu
KALIZA-hauwezi niambia kitu chochote nikakuelewa
KISAMVU-Kaliza unani tena, umefikiri vizuri, 
                  Hii shughuli ya ma'na, akili yapata ari, 
                 Tunapata kujuana, wa Dar na Zanzibari, 

                  Na mengine mengi sana, yenye baraka na kheri, 
                 Vipi uache shairi, sasa unatunga shanga?.
                                                                                     KISAMVU


KALIZA-hapo bado hujanishauri.


KIJAMUNU- Kaliza nakushauri
                   Huko uendako siko
                   Safari yenye dosari

                   Ilojaa masumbuko
                   Kwahitaji ujasiri
                   Kuikwepa baikoko

KISAMVU- Hilo ni jambo la heri, tunga mwanakwetu tunga                    Umeigundua siri, huku hakuko shuwari
                    Watungie wanawari, tena wazidi kuringa

                    Tunga mwanakwetu tunga,

BABA-unasikia wanachosema wenzako au bado tu kichwa chako kigumu,nitakukata kofi (anasimama kwa hasira)

KIJAMUNU-(anasimama na kumzuia baba)baba acha hiyo utakuja kuua bure we mwenyewe unamuona mtoto mwenyewe halivyo.


DOTO-Haya na mtunge nyie, miye nibaki kusoma,
Na sifa niwasifie, japo hamtungi vema,
Kubwa msinichukie, kutunga sasa nakoma.
Maiki niwaachie, mghani zenu nudhuma,
Yanini tugombanie, langu jicho natazama,
Sikio liwasikie, hovyo mnavyo koroma.
Pongezi niwapatie, mzishibe kama sima,
Kiti changu mkalie, Dotto nisimame wima,
Hai msinifukie, kutunga ninasimama.
Chuki msinifanyie, mkome kunisakama,
Yangu sifuatilie, siutaki uhasama,
Ushairi basi mie, sasa naenda kulima.
Khamsa ziwaingie, hizi beti nzimanzima,
Hata kiki mtumie, siyo rahisi kuvuma,
Nilipo mnifikie, tungeni za kusimama.
28 January 2018 Jumapili 10:49 am
                                         Jina la Mtunzi: Dotto Rangimoto
                                         Jina la Utunzi: Jini Kinyonga
                                       +255762845394 Morogoro.
KIJAMUNU-Lakini baba tulisha kwambia toke mwanzo hawa watoto wako umelea vibaya,ona sasa wanavyoanza kuteteana au labda kisa mapacha.
BABA-ni heri ningebadilishana na mifuko ya saruji nimalizie nyumba yangu kuliko hawa watoo eeh.
BACHUWataka nitoa chozi,nikose pa kufutia
Yanitoke makohozi,kebekebe na mafua
Au ugonjwa wa ngozi,chini kugalaukia

Usiache taumia

We ni wangu kiongozi,mwenyewe unatambua
Bachu nipo kwenye kozi,mafunzo najipatia
Pengo siliache wazi,maudhui tapotea
Usiache taumia

BABA-iiiiii (anaanza kutoka machozi kwa uchungu)
KISAMVU-baba nyamaza.
BABA-nimesema sikubali,leo nitajua nani baba na nani mtoto humu ndani.
baba anasimama anaingia chumbani na kutoka na panga.
................JE NINI KITAENDELEA.......................
MKUSANYAJI-Idd Ninga.
                       +255624010160
                       iddyallyninga@gmail.com
WATUNZI-Bachu Bsc
                Dotto Rangimoto Chamchua
                Kaliza Bakari
                  Suleimani Kissamvu 
                 
                 Idd Ninga

Hakuna maoni