Mimba na Kifungo
MIMBA NA KIFUNGO.
Nawaza tu peke yangu, kwa haya yalonikuta,
Tamu imekuwa chungu,mfaume ninajuta,
Niokoe mungu wangu, madhira yaniburuta,
Najiona niko jela, natumikia kifungo.
Mawazo yananituma, nijipeleke mwenyewe,
Tena niwahi mapema, haraka nisichelewe,
Nimwambie wake mama,anayo mimba mwanawe,
Mimi ndiye nilompa,na mimba tahudumia.
Napata wazo lingine, lanitaka nisiende,
Hatonitaja pengine, kwa hekima anilinde,
Ataje mtu mwengine, niiokoke rumande,
Kwa vile nimjuavyo,lazima atanitaja .
Nini nitamdanganya, baba yake akijua,
Alishawahi kunikanya, nimuache Sikujua,
Kwa hiki nilichofanya, dhahiri ataniua,
Najutia najutia, tamaa itaniponza .
Yupo kidato cha pili, na tayari anamimba,
Nijuavyo serikali,macho hawatayafumba,
Nitatafutwa vikali, nikakipande kizimba,
Ni miaka thelathini,hiyo haina dhamana.
Bibi yake ni hakimu, mahakama ya mkoa,
Kesi hizi huhukumu, kwa mfano kuutoa,
Vipi kwangu iwe sumu, nyundo kutoikongoa,
Sinapo pakutokea,yani lazima nifungwe.
Hapa nipo kwenye basi, ninakwenda Takaungu,
Bali nina wasiwasi, naogopa walimwengu,
Nishamwachia Qudusi, anilindie mwanangu,
Ni bora niende mbali, huwenda nikajiponya.
Mshairi Machinga,
mfaumehamisi@gmail.com,
0716541703/0677620312,
Dar es salaam, Kariakoo.
Post a Comment