Ushairi na pesa
USHAIRI NA PESA
MFAUME HAMISI
Nijile kaka nijile, nijile mi mwanagenzi,
Haswaa uniambile, kuhusu hizo zenu tenzi ,
Watu wote wasikile, hadi wale wakufunzi,
Vipi nitapata pesa, kwa fani ya ushairi.
ULAMAA HEMED
Nimeelewa tawile, swali lako nalienzi,
Nisemayo msikile, haswa nyie wanagenzi,
Mana mwapiga kelele, eti hazilipi tenzi,
Ukitaka pata pesa, kwanza tunga tungo nzuri.
MFAUME HAMISI
Jambo hilo si la kweli, na ushahidi naweka,
Wapo watunzi wakali, mithili yake Muyaka,
Hali zao ni dhalili, nasema kwa uhakika,
Kama kutunga ni pesa, mbona hawana dinari?.
ULAMAA HEMED
Umeitoa dalili, wakati si muafaka,
Muyaka kweli ni nguli, kwa ya zamani miaka,
Tungo hazikuwa dili, ili wapate nafaka,
Kwa sasa tungo ni pesa, ila utunge vizuri.
MFAUME HAMISI
Ona wale jamvini, majagina wa kisasa,
Watunga tungo makini, tena zisizo makosa,
Mbona sasa masikini, hakuna mwenye verosa,
Wako wapi wenye pesa?, kwa kutunga mashairi.
ULAMAA HEMED
Mawazo yao ni duni, ingawa watunga hasa,
Tungo za mtandaoni, vipi zitaleta hisa,
Wengi hawana diwani, wamekaa kibubusa,
Kama unataka pesa, jitanagaze mshairi.
MFAUME HAMISI
Haa! wanazo titiri, tena diwani lukuki,
Walo mule ni mahiri, japo hawafahamiki,
Hayalipi mashairi, heri kuimba muziki,
Nitajie wenye pesa, sababu ya ushairi.
ULAMAA HEMED
Kijana acha kiburi, kwanini huambiliki,
Hata yale mashairi, kabla kuwa muziki,
Tatizo mwafanya siri, kutangaza hamtaki,
Dotto ni mfano hasa, Kivuli yupo mahiri.
MFAUME HAMISI
Basi kaka nakubali, ushairi unalipa,
Nitatunga tungo kali, nanyi heko mtanipa,
Ushairi ni amali, ni kweli hujaongopa,
Pesa zitabaki pesa, yatadumu mashairi.
ULAMAA HEMED
Angalau tafadhali, ujinga umekuchupa,
Zimekurudi akili, si mwenye kutapatapa,
Tungo zikiwa jamili, huwezi kutoka kapa,
Kutunga si kujitesa, hapa nasema kwaheri.
Watunzi:
1. Mfaume Hamisi
(Mshairi machinga)
0716541703
2: Ulamaa Hemed
0717 501557
Post a Comment