Ushairi si uzee
USHAIRI SI UZEE
Tuepuke kukariri, muda ushabadilika
Ujuzi wa ushairi, upo kwenye kila rika
Acha nivunje pingiri, watu waliyoiweka
Ushairi si uzee, dhana potofu ondoa.
Ushairi si uzee, dhana potofu ondoa.
Wapo vijana wazuri, mafundi wanosifika
Watungao Kwa urari, shairi likaimbika
Tenzi zao machachari, hazina chembe ya shaka
Ushairi si uzee , dhana potofu ondoa.
Sasa tungo ni titiri, waleo wanaandika,
Zinazovuka bahari, watu wakaelimika
Bara nako zanzibari, watunzi wamemwagika
Ushairi si uzee, dhana potofu ondoa.
Wamo wakongwe hodari, hili linafahamika
Watungiapo habari, msomaji humteka
Pamwe huoni dosari, kama sauti ya dhika
Ushairi si uzee, dhana potofu ondoa.
Yapasa kutafakari, kisha ndio kutamka
Mshairi ni tajiri, wa lugha sio miaka
Atumie umahiri, ujumbe uweze fika,
Ushairi si uzee, dhana potofu ondoa.
Ilikuwa ni dhamiri, ya somo kulipeleka
Jamii ipate kheri, dhana mbaya kutoweka
Wala isiwe shubiri, lengo mkakengeuka
Ushairi si uzee, dhana potofu ondoa.
Mshairi Machinga,
0677620312/0716541703,
Dar es salaam, Kariakoo.
Post a Comment