Header Ads

test

USHAIRI NA SAYANSI,NINGELISOMA SAYANSI



          NINGELISOMA  SAYANSI
Lile neno ningejua, huja mwisho wa safari 
Leo ndio nang'amua,  Shari Kamili si  kheri 
Sina ninachoambua, zaidi ya kusubiri
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Tumejikuta ni wengi, mpaka tuko ziada
Tukaukosa  msingi ,wakuendana na muda
Mfumo hatuukongi, ndomana twapata shida 
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Ningechukua  hesabu,  fizikia  na kemia
Ningekesha na vitabu, kutwa nikijisomea
Nisingeipata tabu,  ya kazi kujipatia
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Ningeshinda maabara, vitendo kuthibitisha
Nikiwapasua vyura, na kisha kuwaponesha
Ningepata kazi bora, yenye pesa za  kutosha
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Sayansi ina nafasi, kwa uchumi wa viwanda
Uwe hata kandarasi, kila uchwao ni tenda
Kwingine ni sarakasi, sio kama ninaponda 
Ningelijua  mapema, ningelisoma sayansi.

Wote  ninawaambia,  mlioko mashuleni
Sayansi kushikilia,mkisoma chimbueni
Msuli kuikazia, msifanyie utani 
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Mkopo  mtaupata, pasipo kipingamizi
Mia mtaziburuta, bila ya vichachawizi
Ajira zitajileta, ziko nyingi wazi wazi
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Shairi nahitimisha ,nishatoa ushauri 
Sijatunga kupotosha,mengine kuyakejeri
Sihitaji kurefusha,  Nikaimaliza ari 
Ningelijua mapema, ningelisoma sayansi.

Mshairi Machinga, 
0716541703/0677620312.
Dar es salaam, Kariakoo.

Hakuna maoni