Header Ads

test

Tabia ya muungwa- Hamisi Kisamvu Mkanyaji


            TABIA YA  MUUNGWANA

Kuno kunena kunena, leo nalinena hili
Nalinena kwa mapana, kwa lugha ya kiswahili
Tabiaze muungwana, si mtu wa ndimi mbili
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.

Nawala hawi mpana, hujiona yu dhalili
Subira imejazana, zimetuwama akili
Kidogo atachovuna, hajipandishi manzili
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.

Ni mbali ametengana, nazo hasira za mali
Hufanya mambo kwa kina, na kukumbuka ayali
Si mambo kujalizana, moyowe huona dhuli
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.

Hasa alo muungwana, si mtamani batili
Uchache kwenye hazina, wala haoni fiili
Hujibanza kwa Rabana, kwa visimamo laili
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.

Na waja atagawana, japo na kiwe kalili
Huwa hapendi kuona, wakinyongeka ahali
Changi ni kuchangizana, hiyo ndioye sabili
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.

Yeye hutafuta Janna, thama kashika adili
Hawi mwenye kujivuna, kwa afanyazo fadhili
Huwa ni mwema msena, kwa matendo na kauli
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.

Hapa tama ya kutona, kalamu yangu mvuli
Wenye macho wataona, hayano yana kulali
Ila walo na hiyana, si lazima kukubali
Kutosheka na akali, tabia ya muungwana.


MKANYAJI
HAMISI A. S KISSAMVU
0715311590/0784311590
kissamvujr@ gmail.com
    .   kutoka
     (Baitu shi'ri)
    DAR ES SALAA

Hakuna maoni