SIKU MOJA NITAKUA
SIKU MOJA NITAKUA
Mimi nitakapokua, nitauacha utoto
Mazuri nitayajua,mepesi pia mazito
Hatamu nitachukua, kukitafuta kipato
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara .
Hekima nitatumia, nayo lugha ya mvuto
Ugomvi kuuamua, pasipo wapo majuto
Watu sitawabugua, wazee wala Watoto
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara.
Nyumbani sitakimbia, kuelekea maputo
Kiwanja nitanunua, Mjini gongolamboto
Niishi na familia, ndugu, mke na mtoto
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara.
Vijana nitawaasa, wafanye yalioyo mema
Waziepuke anasa,watende vitendo vyema
Na waitafute pesa ,kwa njia ilo salama
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara.
Nitahamasisha sana, watu waifanye kazi
Usiku nao mchana, wakitumia ujuzi
Wasilete kujuana, wakazaa ubaguzi
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara.
Uhalifu sitafanya, kumsumbua yeyote
Pesa, mali kupokonya, au kuiba chochote
Wala sitakua panya, vitu vyao niving'ate
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara.
Kaditama nimetua, sio kwamba yameisha
Yapo ya kusimulia, ila leo yanatosha
Siku hiyo nikikua, ukweli sitapotosha
Siku moja nitakua, nitafanya ya busara.
Mshairi Machinga,
0716541703/0677620312,
Dar es salaam, Kariakoo.
Post a Comment