Header Ads

test

Nakukumbuka Mwendani





Mtunzi: Jane Davis
WhatsApp +255657360750
jmwanizuwa@gmail.com 

Ni usiku wa manane Edna anashtuka kwenye njozi,anafikicha macho kisha anatizama kalenda..Ooh taratibu anatokwa machozi,akiimba"Suley mpenzi nilikupenda,siku zote sikujuwa wewe ni tozi, umeamua kunitenda,ukisema sijui mapozi.Sawa Baba nenda nenda,fuata weupe wa ngozi.

Suley umesahau kabisa mimi nawe tulikotoka,kule kijijini kwetu Sumbawanga.Hukumbuki namna ulivyokuwa umechoka,na maisha ya kutangatanga.Ngozi kavu iliyopauka, kichwani ukoko unatoa unga.Leo umeamua kunigeuka,hadi kuniita mimi danga!!! Unashuka unashuka, unaniita mimi mwanga.Ooh kumbe nilikurupuka,kukata nyanya na panga.Na sasa ndio nashtuka,kweli najiona mjinga.Na kumbe nilifuga joka,nisiloweza kulifunga."

Ghafla rafiki yake anaamka na kumsihi alale,Edna analala lakini sio usingizi.Macho yake yanabaki yakitalii juu ya paa huku kichwani mawazo tele yakimzonga.Kumbukumbu za tukio la nyuma zinamrejea,anaanza kukumbuka...

"Kuanzia leo wewe sio mke wangu,tena toka nenda kadange huko"


"Suley mpenzi wangu nini kimekupata,mbona sielewi?"


"Huelewi eeh!,nasema hivi sikutaki tena .Naomba uondoke Edna siwezi kuwa na mwanamke mshambamshamba kama wewe."

"Lakini mpenzi wangu mbona hivyo,unanifukuzaje nyumbani kwangu?"

"Una kwako wewe? Hebu toa kiwingu mchawi mkubwa wewe,Precious baby hilo ndio janamke nilikuwa naishi nalo"

Kumbukumbu ya malumbano kati yake na mpenziwe Suley inamuumiza sana na kuibua kilio cha kwikwi. 


Wapenzi hawa wawili ama niseme Mke na mume walikutana Sumbawanga miaka mitatu nyuma.Suley akiwa anatokea Tabora almaarufu kama Mboka,baada ya kutafuta kazi kwa muda mrefu ndipo alipokutana na Edna.

Wakati huo binti alikuwa kijijini kwao kusalimia na kutafuta kijana wa kumtembezea mayai jijini Daresalaam.Hiyo ikawa bahati kwa Suley,waliondoka kurejea jijini na kuishi pamoja.

Mazoea ya hapa na pale mara penzi likachipua,Edna aliyekuwa akijishughulisha na biashara ya mgahawa alimpenda na kumjali sana Suley hadi wazazi wake huko Tabora.Alimpa mbinu mbalimbali za biashara,akamuunganishia kazi kwenye shirika la wazungu.Akawa akilipwa mshahara mnono, maisha yakawanyookea ndani ya miaka miwili tu Suley alikuwa kama bosi,alinenepa na kuwa bonge la handsome tishio kwa warembo.

Hapo ndipo mwanaume yule alikengeuka na kuanza kumnyanyasa Edna.Ikafika wakati akamtolea mkewe mabegi yake nje na kumfukuzia mbali.Hakumpa chochote zaidi ya nguo,hilo likawa pigo kwa Edna huku ikiwa furaha kwa Suley na mpenziwe Precious.


Ulikuwa ni mwaka mgumu kwa Edna, msongo wa mawazo haukumuacha.Mara kadhaa alijaribu kujitoa uhai lakini aliokolewa.Rafiki yake kipenzi Theresa alimchukua hadi Mwanza,binti yule alisimama kidete akifanya hili na lile,kumpeleka kwa wanasaikolojia,kumtoa out na kumjenga kiimani.Juhudi zake hazikupotea bure zilileta matokeo,Edna alikaa sawa akaanza na biashara ya vitafunio nje ya shule moja ya msingi.


Mara tu baada ya kuachana na Edna, Suley akawa ni mtu wa starehe tu,hakuna viwanja ambavyo hakuingia.Precious alimshauri aache kazi ili asimamie vizuri biashara, mapenzi upofu Suley aliridhia na kuacha kazi.

Kutokana na kuwa hakuwa mzuri kwenye mahesabu alijikuta akitumia zaidi kuliko kuingiza.Na katu hakuliona hilo aliendeleza ufujaji.


Kwa bahati mbaya siku moja akirejea nyumbani usiku ,kutokana na kulewa sana alisababisha ajali.Ajali iliyomfanya avunjike mguu na mkono.


Alilazwa hospital miezi miwili,na ndani ya siku zote hizo hakupata kumuona mpenziwe Precious.Huduma zote alipatiwa na rafiki zake ambao nao hawakufahamu ni kwa nini binti haonekani hospital.


Hatimaye Suley aliruhusiwa kurejea nyumbani, moyoni alikuwa na furaha kwamba anakwenda kupumzika.Lakini furaha hiyo ilikata mara tu alipofika nyumbani na kushuhudia jambo asilolitarajia.


Geti liliegeshwa na milango ilikuwa wazi huku ndani kukiwa kweupe mithili ya uwanjani.Majirani walimshangaa alipowaulizia huku wakimwambia waliona Fuso ikipakia mizigo wakahisi wanahama kimyakimya.


Suley alianza safari hadi kwenye fremu yake ya biashara,nako palikuwa patupu.Chozi lilimdondoka mtu mzima hakutaka kuamini Precious kaondoka na kila kitu.

Alihisi kuchanganyikiwa hata alipoomba hifadhi kwa rafiki zake,kila mtu alimwambia hana nafasi.

Alikata shauri kusafiri hadi Mwanza nyumbani kwao Precious maeneo ya Usagara ambako alielekezwa na rafiki mmoja wa mpenziwe.


Baada ya kufika Mwanza juhudi za kumpata Precious ziligonga mwamba.Suley na ugeni huko akawa akizulula kuombaomba tu,asingeweza kufanya kazi ngumu kwani mguu wake haukuwa  umepona vizuri.


Maisha yakawa magumu kwake alichojitahidi ni kuzunguka kwenye vibanda vya chips na kumenya viazi kwa ujira mdogo. Mawazo mengi yakamfanya aanze kulewa na kuvuta sigara.Kila pesa aliyoipata aliipeleka kwenye pombe huku akisahau Kabisa kuhusu chakula.


Ulevi ule haukumpenda mwili wake ulianza kudhoofu kwa kasi ya ajabu.Ngozi ikampauka,mgongo ukampinda zikamtoka na mbavu.


Siku moja Edna akitoka shuleni kuuza vitafunio,kwa mbali aliwaona wanafunzi wakimshambulia mtu.Mtu aliyeonekana kama mlevi alinyanyuka na kuondoka huku akipepesuka.


Mara karatasi jeupe aliloshika mkononi mtu yule lilimponyoka likapeperuka hadi chini ya miguu ya Edna.Binti yule alitaka kulipita lakini karatasi lile lilifunuka upande wenye maandishi.


Shauku ya kutaka kuyasoma ikamvaa,akaiokota karatasi ile na kuanza kuisoma,lilikuwa ni shairi likisomeka sawia....


"Kwako Edna,

NAKUKUMBUKA MWENDANI.

U mwanamke wa shoka,ua lililochanua.
Ni mbali tulipotoka, hakuna asiyejua.
Nakukumbuka mwendani, rejea tuwe pamoja.
Hadi kwa wazazi Mboka,wote wanakutambua.

Tangu ulipoondoka,uzito nimepungua.
Mwili umekongoroka,nimebaki kama bua.
Furaha yanitoroka, sonona ninaugua.
Nakukumbuka mwendani,rejea tuwe pamoja.

Kwako nilitononoka, mwili nikajitanua.
Chini nilipodondoka, nyonda ulininyanyua.
Nilipohisi kuchoka,ulinipiga kifua.
Nakukumbuka mwendani,rejea tuwe pamoja.


Vile alivyoumbika,zuzu akanizuzua.
Kwake nikapaparika,lako penzi kuliua.
Najuta kuhadaika,mali amenikwangua.
Nakukumbuka mwendani, rejea tuwe pamoja.

Sasa nimebadilika,ujana nimeutua.
Nisamehe malaika,kosa nimeligundua.
Sitokutenda hakika, kwenye jua na mvua.
Nakukumbuka mwendani,rejea tuwe pamoja.

Edna baada ya kumaliza kusoma shairi lile alianza kukimbia huku na kule kumtafuta Suley. Mbele kidogo kwenye barabara ya lami aliona umati mkubwa wa watu wakitizama jambo.


Anauliza huku mapigo ya moyo yakiwa kasi.

" Kuna nini?"


"Kuna mtu kapita hapa kama kachanganyikiwa vile,akajirusha kujilengesha kwenye gari ikiwa kasi imemgonga kafariki hapo hapo"


"Suley!!!!!"


MWISHO

 

Hakuna maoni