Mahari mloitaja ni hatari kwangu
MAHARI MLIYOTAJA
Lo! sitaki natamka, bila jicho kupepesa,
Hakika nimechemka, bora mke kumkosa
Nakubali kuumbuka, heri niitwe garasa
Mahari mliyotaja , kuilipa sitaweza.
Hali yenyewe masika, mfukoni sina pesa
Ni wazi ninaropoka, najuta kuleta posa
Sijali mkinicheka, nakubali nimenasa
Mahari mliyotaja, kuilipa sitaweza.
Si baba wala si kaka, mwenye hao ng'ombe tisa
Mama mshona mikeka, dada mcheza kibisa
Nami mziba viraka, mbona mnatunyanyasa?
Mahari mliyotaja, kuilipa sitaweza.
Ni vingi mlivotaka, vingine ni vya anasa
Mkaja ,suti ,mashuka, mbuzi kumi wa kisasa
Majembe, panga, na shoka, mchumba ninamsusa
Mahari mliyotaja, kuilipa sitaweza.
Kanga, pombe kadhalika, mmenitoa hamasa
Kwa hilo sijarizika, Kwa huo wenu usasa
Na mbio nazitimka, ya nini kuweka hisa
Mahari mliyotaja, kuilipa sitaweza.
Kinyonge nasononeka, naimaliza kurasa
Mipango imetoweka, ya kumuoa Hamisa
Machinga ninaondoka, nimeshafikisha kisa
Mahari mliyotaja, kuilipa sitaweza.
Mshairi Machinga,
+255677620312/+255716541703,
Dar es salaam, kariakoo.
Post a Comment