Naikumbuka Morogoro-ujumbe maridadi kwa mshairi nguli wa kiswahili toka nchini Rwanda.
NAKUMBUKA MAROGORO, VIKINDU NA MIBURANI.
********************************
1.
Namshukuru Karima, Hadi leo kuniweka,
kaniwezesha kusema, tamko hini mwafaka.
Ni la kheri na salama, na shehena ya baraka,
kwa wenyeji wa Vikindu, Marogoro, Miburani.
2.
Alfu moja mia kenda, aruba wa themanini,
Marogoro nilienda, kuwa mwalimu shuleni.
Madogo nikawafunda, pale pale kijijini,
ninaikumbuka shule ya Msingi Marogoro.
3.
Temeke basi n'kipanda, Mbagala nilishukia,
kwa mguu nikaenda, na Vikindu kufikia.
Niliendelea kwenda, maporini kupitia,
kwelekea Marogoro, kwenye yangu masikani.
4.
Ikifikia jioni, ndo Vikindu ninatuwa,
kwendelea safarini, hatarini ningekuwa,
simba wakiwa njiani, kuwinda vilochelewa,
nalitafuta malazi, maeneo ya Vikindu.
5.
Marogoro kijijini, sana nilikuzowea,
hadi ndani viungani, kwa wakwezi n'kitembea.
Salamu zipokeeni, na dua nawaombea,
wenyeji wa Marogoro, Vikindu na Miburani.
6.
Tena nikahamishiwa, kwingine kufundisheni,
shule hiyo ilikuwa, ya msingi Miburani.
Zaidi nikaelewa, maeneo ya Pwani,
Kiswahili kulikoni, Mola kujazie kheri.
7.
Sikudumu Miburani, n'kendelea Mzizima,
ni'kotulia jijini, ndani ya Darisalama.
Swahiba wangu mwendani, simsahau daima,
ni Idd bin Mdede, Keko alinipokea.
8.
Ndani ya Keko Torori, ku kiwanda cha sabuni,
Idd rafiki mzuri, kanizoweza yakini.
Bin Mdede u kheri?, huko uliko jijini?
leo ninasikitika, kuwa tumepoteana.
9.
Nayakumbuka mandhari, ya viunga vya minazi,
mdundiko nakumbuka, ngoma swafi ya wakazi.
Ingawa nimekutoka, kukusahau siwezi,
nakumbuka Marogoro, Vikindu na Miburani.
10.
Beti kumi ninatuwa, Shukurani Maulana,
dukuduku nimetowa, kwa tungo hini mwanana.
Nakuomba majaliwa, tena n'kuzuru Rabana,
nakumbuka Marogoro, Vikindu na Miburani.
*******************************
Rwaka rwa Kagarama, Mshairi Mnyarwanda.
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,RWANDA.
Post a Comment