SOMO-Madhara ya ndugu kuchukiana.
Ndugu wasiopendana, huwa wananishangaza,
Haswa wanapokanana,huku wakijiapiza,
Tena wakitukanana, na maneno ya kubeza,
Ndugu wasiopendana, kuna siku hujutia.
Yaani wawezakuta ,wametoka tumbo moja,
Ila wanavyojisuta, utaviona vioja,
Wanapelekana puta, kuvunja wao umoja,
Ndugu wasiopendana, kuna siku hujutia.
Vibaya upangiana, kamwe wasisemezane,
Vijembe kurushiana, na kurogana pengine,
Vivyo wakiambiana, wakifa wasizikane,
Ndugu wasiopendana, kuna siku hujutia.
Mmoja akiugua, nduguye hufurahia,
Mola akimchukua, aliyebaki ulia,
Kilio hukiangua, pamwe na kugugumia,
Ndugu wasiopendana, kuna siku hujuitia.
Mazikoni anakwenda, huku moyo waungua,
Ndugu asiyempenda , hayuko chini ya jua,
Chuki waliyoipanda, vipi wataifungua?,
Ndugu wasiopendana, kuna siku hujutia.
Kalamu naidondosha, bali ndugu pendaneni,
Ujumbe wangu watosha, kazi kaufanyieni,
Udungu hadhina tosha, jambo hilo eleweni,
Ndugu wasiopendana, kuna siku hujutia.
Mshairi Machinga,
mfaumehamisi@gmail.com,
0716541703/0677620312,
Dar es salaam, kariakoo.
Post a Comment